Habari Kitaifa

Dkt MAGUFULI: Ole wenu Mnaopotosha Takwimu Sahihi

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi kwenye jengo  la Ghorofa nne la Ofisi za  Taifa za Takwimu zilizopo Mkoani  Dodoma huku akionya vikali watu wanaompotosha takwimu na kuwatisha watanzania.

Rais Magufuli amesema, wapo watu kwa makusudi kabisa wamekuwa wakiupotosha umma juu usahihi wa takwimu mbali mbali za nchi bila kuwa na vyanzo sahihi vya takwimu ambao ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

“Mmesikia wenyewe hapa tumekuwa namba mbili kwa ubora wa takwimu katika nchi za Afrika, tukitanguliwa na Nchi ya Afrika Kusini, ametuambia mkurugenzi mkuu wa Takwimu Mama Chuwa, lakini wapo watu wengine sijui takwimu zao wanazitoa wapi na kuwadanganya wananchi” alisema Dkt. Magufuli.

Rais Magufuli ameiagiza Ofisi ya Taifa ya takwimu, kuitumia ipasavyo sheria ya takwimu namba 37 ya mwaka 2015 kifungu kupitia kifungu kidogo cha 3 hadi cha 5 ambacho kinawalenga wapotoshaji wa takwimu na kwakutumia kifungu hicho basi mtu anaweza kufungwa kati ya miezi sita hadi miaka mitatu au faini ya kati ya Mil. Moja hadi 10 au vyote kwa pamoja.

“Vyombo vya habari, Watu wa Mitandao, tusitafute takwimu zakupika tafuteni takwimu sahihi kutoka vyanzo sahihi” amesema Rais Magufuli na kuongeza kuwa, Maendeleo katika Nyanja zote hutegea takwimu sahihi.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya taarifa ya takwimu Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Taifa ya Takwimu Nchini Dkt. Albina Chuwa, alisema mpango uliopo mbele yao ni uboreshaji wa majengo, kusomesha wataalam, lakini pamoja na kuweka viwango bora vya ukokotoaji wa takwimu.

“Mhe. Rais tunajenga Jengo la Ghorofa moja pale mkoani Kigoma, nikuhakikishie kupitia wadau wetu wa maendeleo jengo hilo tutalikamilisha bila kuhitaji msaada wa serikali” alisema Dkt. Chuwa.

Chuwa amesema, mbali na kuendesha sensa ya taifa tangu mwaka 1967 wakati wa watanzania walipokuwa Mil. 13, Ofisi yao pia imeendelea na zoezi la sensa ya watu na makaazi kwa miaka tofauti na mwaka wa mwisho kufanya sensa 2012 watanzania walikuwa Mil. 45, huku akitoa makadiri ya watu Mil. 60 na zaidi ifikapo wakati wa Sensa ya 2022

Awali kabla yakumkaribisha Mh. Rais, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, alimwambia Mh. Rais kuwa wanawashukuru sana wadau wa maendeleo kwa jinsi wanavyozidi kushirikiana na Nchi ya Tanzania katika shughuli za maendeleo hasa  Benki ya  Dunia.

“Mhe. Rais kazi kubwa unayoifanya, wenzetu (World Bank) na wadau wengine wa Maendeleo wanaithamini sana na ndio maana wamekuwa bega kwa bega katika shughuli za Maendeleo alisema Mpango na kuongeza kuwa jengo linalojengwa Dodoma ni la pili, jengo la kwanza lipo Zanzibar na linategemewa kuzinduliwa mapema mwaka ujao.

Mbali na kufanya shughuli ya uwekaji wa jiwe la Msingi Mh. Rais hakusita kuongelea mambo mbali mbali yanayo husu uchumi wa nchi na kusema kuwa uchumi wa nchi umekuwa kwa kiwango cha aslimia 6.8 huku mfumuko wa bei ukishuka na kufikia asilimia 4.4 ambapo Tanzania imeongoza katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na uchumi unaokuwa vizuri na kuwa miongoni mwa Nchi 5 zinazofanya vizuri barani Afrika katika suala la Ukuwaji wa Uchumi.

Akihitimisha Hotuba yake Mhe. Rais amezitaka taasisi zote nchini kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Bodi ya Taifa ya Takwimu ili kazi wanayoifanya iwe na ufanisi, huku akimuagiza Waziri wa Fedha kufatilia suala la Airtel kwani inaonesha kampuni hiyo ilikuwa mali ya TTCL.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *