Habari Kitaifa

ATE:Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka” inatambua Waajiri bora na Mchango wao

on

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimetoa Tuzo ya  Mwajiri Bora wa  Mwaka  2017 lengo likiwa ni kutathimini mchango wa  rasilimali watu ili kuwawezesha  kushiriki   kikamilifu katika utendaji wa masuala  mbalimbali ya kibiashara.

Akizungumza katika sherehe za  utoaji  wa Tuzo hizo Waziri wa Nchi  Ofisi  ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira  na Wenye Ulemavu Bi. Jenista  Mhagama  aliyemwakili Waziri Mkuu, amesema kuwa amefurahishwa jinsi ATE walivyowajali Sekta nyinginezo na kuongeza baadhi ya Tuzo ambazo  hazikuwepo awali.

“Nimefurahishwa sana na ATE  kwa kujali na kuamua kuongeza Tuzo nyingine mpya 12 ikiwemo ya  Tuzo ya Mwajiri Mzawa, hii inaonyesha kuwa mnajali Sekta nyinginezo na mnastahili pongezi kubwa  sana” alisema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE)  Bi. Jayne Nyimbo ameeleza kuwa wameendelea kutoa mafunzo katika maeneo muhimu hasa katika sheria za kazi na  usimamizi wa rasilimali watu ili kuhakikisha tunadumisha utulivu, amani na kuongeza tija sehemu za kazi.

“Napenda kuwakumbusha wanachama wetu na  waajiri wote nchini kuendelea kutumia huduma zetu ili kuongeza  tija na ushindani, waajiri tunatambua juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini” alisema Bi. Nyimbo.

Aidha aliongeza kuwa  waajiri  wote wangependa mgawanyo mzuri wa tozo  ya  kuendeleza ujuzi  mahala pa kazi  (SDL) ili yote iende  kugharamia mafunzo ya ufundi stadi  na  siyo kwenda  kwenye mikopo ya  elimu ya juu  na kwa  kufanya hivyo itasaidia sana katika ujenzi wa Tanzania ya Viwanda.

“Hatuwezi  kwenda kwenye uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda kwa jinsi sheria za kazi zilivyo ambazo zinatetea uzembe, ubadhirifu, tunakubali kama waajiri sheria zilinde haki za wafanyakazi lakini zisiwatetee wafanyakazi wabadhirifu, wazembe  na  kadhalika” alisema Bi. Nyimbo

Naye Mkurugenzi Mtendaji  wa Chama cha Waajiri  Tanzani, Dkt. Aggrey Mlimuka  alisema kwamba tuzo ya mwajiri bora wa mwaka ilianzishwa mwaka  2005  ambapo  ililenga zaidi kuwatambua wanachama  waliofanya vizuri katika  kuweka mikakati  bora  yenye kuthamini usimamizi wa rasilimali  watu  na shughuli za kibiashara.

Dkt. Mlimuka aliongeza  kwa miaka kadhaa tuzo hizi  zimehamasisha makampuni, wanachama kuweka juhudi katika masuala ya ajira na usimamizi wa rasilimali  watu kama  mkakati wa  kuwezesha makampuni yao  kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, furaha, ushindani na yenye kushiriki kikamilifu katika kuongeza tija na ushindani.

 

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *