Habari Kitaifa

CUF yathibitisha kuhama Kwa aliekuwa Mbunge wake Maulid Mtulia

on

Chama cha Wananchi (CUF) leo kimethibitisha na kutoa ufafanuzi kuhusu kujivua uanachama na kuachia nyadhifa zake zote na kukihama chama hicho kwa aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia na kutangaza kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma Abdul Kambaya amesema kuwa Maulid Mtulia ameondoa uaminifu kwa wanachama wa Jimbo la Kinondoni kwa madai ya kuwa wananchi walimwamini kulala nje wakipigania kura zake za ubunge huku wengine wakiumizwa na kufikishwa mahakamani lakini yeye amewasaliti.

“Mtulia aliwania udiwani wa Kata ya Ndugumbi mwaka 2005 akashinda kura za maoni lakini baadaye akajitoa, ikabidi niingie mwenyewe kugombea ili niokoe jahazi, mwaka 2015 alijaza vibaya fomu ya kugombea ubunge, akaondolewa kwenye mchakato, tulipambana hadi akarudishwa na Tume ya Uchaguzi ili agombee, hii yote inaonyesha namna gani alikuwa amejiweka sokoni mwenyewe” alisema Kambaya.

Aliongeza kuwa Mtulia amekitia doa chama chao kutokana na matendo yake aliyoyafanya kwa wananchi na chama kwa ujumla huku akisema kuwa kuhama kwake chama kwa madai yake kuwa nikutokana na kwamba anamuunga mkono Rais hayana mashiko hata kidogo.

“Hoja ya kusema anamuunga mkono Rais Magufuli haina mashiko, alichokifanya Maulid ni kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi na sio Rais, kama amemuunga mkono Rais Magufuli, siku kiongozi huyo akimaliza muda wake atarudi tena CUF?” alihoji Kambaya.

CUF imetoa tamko leo ikiwa ni siku moja tangu Mtulia atangaze uamuzi huo ambapo alisema ameridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli hivyo haoni haja ya kuendelea kuwa mpinzani na  hivyo ni bora akamuunga mkono Rais Magufuli.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *