Habari Kitaifa

Dkt. Kalemani Awasha Umeme Maguzo Mawili na Kijiweni mkoani Kilimanjaro

on

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameendelea kuzindua upatikanaji wa huduma ya umeme katika vijiji mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu  (REA III) unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akiwa mkoani Kilimanjaro alizindua huduma hiyo katika Kijiji cha Maguzo Mawili wilayani Same na Kijiji cha Kijiweni wilayani Siha pamoja na kukagua kazi ya usambazaji umeme inayoendelea katika vijiji mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Akiwa katika  Kijiji cha Ndungu wilayani Same, alimwagiza Mkandarasi anayesambaza umeme kijijini hapo kuhakikisha kuwa anawasha umeme katika kijiji hicho ndani ya Siku Saba  na kuhakikisha kuwa umeme huo unasambazwa katika vitongoji vyote vya Kijiji cha Ndungu.

Aidha, akiwa katika kijiji cha Ngarenairobi wilayani Siha na Kisiwani wilayani Same, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa TANESCO kuhakikisha wanafungua vituo vya kutoa huduma kwa wananchi ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

” Serikali ina magari, Pikipiki na vitendea kazi  ambavyo vitawawezesha kuwafikia hawa wananchi na kuwapa huduma, hivyo tuwaondolee adha ya wao kusafiri kufuata huduma pale tulipo bali sisi tuwafuate wao,” alisema Dkt Kalemani.

Vilevile, Dkt Kalemani aliwapongeza watendaji wa TANESCO mkoani Kilimanjaro kwa kufungua zaidi ya vituo 35 vya kuhudumia wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani humo suala linalopeleka wananchi hao kupata huduma kwa haraka.

Kuhusu mradi wa  REA III, mzunguko wa kwanza ambao utakamilika Juni, 2019, Dkt Kalemani alisema kuwa mradi huo unahusisha zaidi ya vijiji 3559 nchini na katika mkoa wa Kilimanjaro, takriban vijiji 83  vitafaidika ikiwa ni pamoja na vitongoji vyake.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Staki, Mbunge wa Jimbo la Siha, Godwin Mollel na Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango Malecela.

Pamoja  na kupongeza kazi ya usambazaji umeme vijijini, Viongozi hao, waliishauri Serikali kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini ili vijiji vingi vifikiwe na huduma hiyo ndani ya muda uliopangwa.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *