Makala

DKT. Kigwangalla Awashukia Viongozi Wanaotaka Kufutwa kwa ya Hifadhi

on

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa hatajibu maombi yoyote yaliyowasilishwa ofisini kwake kutoka kwa  Wakuu wa mikoa, Halmashauri pamoja na  Wakuu wa wilaya  ya kufuta  maeneo ya Hifadhi ili maeneo hayo  yaweze kutumika Kwa ajili ya  matumizi mengine.

Amesema kuwa maeneo hayo yalitengwa kisheria na yana umuhimu mkubwa kiuchumi na kijamii hivyo lazima yaendelee kuhifadhiwa kwa ajili ya faida ya  kizazi cha sasa na kijacho na katika kipindi  cha Uwaziri wake hatajibu ombi lolote lile linalohusu kubadili matumizi ya maeneo hayo kwa vile kuwa na misitu sehemu za mijini ni sehemu ya maendeleo.

Aliyasema hayo jana  mjini Iringa wakati alipokuwa akizungumza  kwa mara ya kwanza na kamati ya kitaifa ya ushauri wa misitu iliyokutana kwa ajili ya kufanya kikao chake cha tatu tangu ilipoundwa mwaka jana ikiwa pamoja na kutembelea msitu wa Hifadhi wa kihesa Kilolo uliiombwa na uongozi wa mkoa kufutwa ili upate kutumika kwa kuweka miundo mbinu mipya ya mji wa kitalii.

Katika kikao hicho ambacho Mkuu wa mkoa wa Iringa, Bi. Amina Masenza alishiriki, Waziri Kigwangalla  alimuomba Mkuu huyo wa mkoa awafikishe ujumbe wakuu wa mikoa wengine ambao walituma na wanaotarajia kutuma maombi ya namna hiyo kuwa yeye  hatakaa ayajibu hadi pale tu yule  aliyemteua ampe maelekezo na si vinginevyo.

Amesema kuwa  Halmashauri nyingi nchini kila zikiona maeneo ya Hifadhi zimekuwa zikifikiria kubadili matumizi ya  maeneo hayo ili yatumike kwa shughuli zingine za maendeleo kama vile  kupima viwanja  ili  kuwauzia wananchi kwa lengo la kukusanya mapato.

“Ofisini kwangu kuna  maombi mengi mno ambayo hata sielewi nianze na lipi na niache lipi, nasema sitajibu ombi lolote lile” alisema Dkt. Kigwangalla.

Aidha, Dkt. Kigwangalla mara baada ya kuzungumza na kamati hiyo alitembelea eneo la hifadhi ya msitu huo  huku  akiwa ameongoza na kamati hiyo  pamoja na uongozi wa mkoa huo na kuwashukia viongozi wa Halmashauri  kwa kuanzisha dampo   katika  eneo hilo  huku kamati ikijionea magari matatu ya taka  yakiendelea kumwaga uchafu kwenye eneo hilo jambo ambalo ni  kinyume na sheria za uhifadhi.

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Japhet Hasunga  aliwashukia watendaji wa mkoa huo  wakati  walipokuwa  wakipishana kutoa maelezo kuhusiana na mipaka na matumizi ya eneo hilo endapo Wizara  itaridhia ombi lao la  kubadili matumizi ya eneo hilo.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Amina Masenza  alimuhakikishia Waziri kuwa eneo hilo endapo watapewa litatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Waziri Kigwangalla mara baada ya kutembelea eneo hilo wakati akitoa majumuisho yake, Alisema kuwa kufuatia ziara hiyo anasubili ushauri utakaotolewa na kamati ya kitaifa ya msitu ndipo atakapokuwa na  jibu kuhusiana na ombi  la kubadilia matumizi la eneo hilo na kuagiza ofisi ya Mkuu wa mkoa kuhakikisha kuwa  maeneo ya  milima kwa vile sio moja ya  maeneo ya hifadhi  yaongezwe katika eneo la hilo  lengo   likiwa ni kuzuia uharibifu wa uoto wa asili unaoendelea katika maeneo hayo.

Awali,  Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati akitoa neno la shukrani alimhakikishia Waziri kuwa watamshauri jambo lolote lile  linalohusu misitu bila kujali litamfurahisha au litamuudhi, kitakachoangaliwa hapo  ni maslahi mapana ya taifa.

Katika hatua nyingine ,Waziri Kigwangalla ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kuanza kuweka nguvu nyingi katika kuhifadhi misitu baadala ya kuvuna na kufanya biashara ya mazao ya misitu  licha ya kuwa TFS imekuwa ikifanya vizuri katika baadhi ya maeneo  lakini katika suala la kuhifadhi misitu imekuwa kama vile sio kazi yake yenyewe kazi yake imekuwa  ni  kuvuna kilichopandwa, kuuza na kukusanya mapato yatokanayo na mazao ya misitu.

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla amesema Wizara inakusudia kuchukua misitu yote iliyo chini ya vijiji na Halmashauri kwa vile zimeshindwa kuisimamia ipasavyo na hivyo kupelekea sehemu kubwa ya nchi kugeuka kuwa jangwa.

Mbali na hilo amewaonya wananchi wanaowazuia watendaji  kuweka vigingi katika mipaka ya hifadhi, huku wengine wamekuwa wakivingoa na wengine kuhamisha vigingi hivyo kutoka eneo moja hadi jingine kuwa  waache tabia hiyo moja la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

About Habari360_TZA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *