Habari Kitaifa

Kigwangalla azindua Kamati Maalumu ya “Urithi wa Taifa la Tanzania”

on

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amezindua kamati ya kitaifa ya kuandaa Mwezi maalumu wa maadhimisho ya Urithi wa Taifa la Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Dkt. Kigwangala amesema anawapongeza  wajumbe wote wa Kamati ya Maadhimisho wa Mwezi wa Urithi wa Tanzania kwa kuteuliwa kwao kwa ajili ya shughuli hii muhimu katika kuhimiza urithi wa Tanzania kwa maendeleo ya sekta ya utalii katika Taifa letu.

Amesema sekta ya utalii imekuwa mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi  wa Tanzania ambapo kwa mwaka 2017 sekta ya  utalii imechangia dola za kimarekani bilioni 2.1 takribani asilimia 25  ya  fedha za kigeni, na kusema kuwa Kamati hiyo itakuwa na wajumbe wateule kadhaa wakiwemo pia Wakuu wa Mikoa ya Arusha, Iringa, pamoja na Simiyu wa itakuwa na shughuli ya kuandaa maandalizi ya Mwezi Maalum wa Maadhimisho ya urithi wa Tanzania.

“Hata hivyo, mpaka sasa sekta ya utalii Tanzania imekua ikijikita zaidi katika utalii wa wanyamapori ili kuvutia watalii ambapo takriban asilimia zaidi ya 80 ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Tanzania bara huja kuona wanyamapori Nchi yetu imejaliwa kwa kuwa na rasilimali mbalimbali za urithi wa Taifa nje ya zile za wanyamapori. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaliwa kuwa na rasilimali za kipekee duniani zinazobainisha harakati za maendeleo ya binadamu kama vile chimbuko lake, teknolojia alizotumia” aliongeza Dkt. Kigwangalla.

Aidha Dkt. Kigwangalla amesema namna ambavyo binadamu amekuwa akitumia mazingira yake ili kumwezesha kuishi kwa zaidi ya miaka milioni tatu iliyopita. Mfano wa rasilimali hizo ni masalia ya Binadamu wa Kale (Zamadamu) walioishi Bonde la Olduvai zaidi ya miaka milioni 1.7 iliyopita na nyayo za Zamadamu aitwaye Australopithecus afarensis aliyeishi Laetol miaka milioni 3.6   iliyopita.

Dkt.Kigwangala amesema kutokana na kuona hayo yote wizara yake imeamua kuwepo na mwezi maalumu kwa ajili ya kusheherekea Urithi wa Taifa la Tanzania, “Kwa kutambua umuhimu huo,kuuenzi, kuutangaza na kuutumia urithi wa Taifa la Tanzania kama kivutio cha utalii na kumbukumbu za Taifa, wizara yangu imeona ni vyema kuwepo na mwezi  maalumu wa kusherehekea Urithi wa Taifa la Tanzania (Tanzania National Heritage Month), tumekubaliana mwezi huo utakuwa ukiadhimishwa kila ifikapo Septemba ya kila mwaka”aliongeza Dkt. Kigwangalla.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *