Habari Kitaifa

DKT. Ndugulile: Watoto Tambueni Haki na Wajibu Wenu

on

Watoto wa Tanzania wamehamasishwa kutambua Haki na wajibu wao katika jamii  kwa kuhakikisha wanazijua na kuzidai haki zao za msingi na kutimiza wajibu wao kama watoto katika jamii.

Hamasa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la Watoto wa Mkoa huo na kuzindu rasmi Baraza hilo.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa watoto wanatakiwa wasikae kimya pale wanapoona haki zo hazitimizwi bali wachukue hatua ya kutoa taarifa katika ngazi husika ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wanaowanyima watoto haki zao.

Naibu Waziri Dkt. Ndugulile amezianisha Haki za Mtoto kuwa ni Haki ya Kuishi, kuendelezwa, Kulindwa, Kushirikishwa na Kutobaguliwa.

Ameongeza kuwa Mabaraza ya watoto yana umuhimu mkubwa katika kuwajenga watoto katika maadili mema na kuijenga jamii ijayo hivyo Mikoa na Halmashauri hazina budi kuyalea na kuyasimamia mabaraza hayo kwa mstakabali wa maendeleo ya Mtoto na taifa.

Amesisitiza kuwa Mabaraza hayo pia yanaweza kutumika kama sehemu muhimu ya kutoa elimu  ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa mimba na ndoa za utotoni ambavyo vinawakumba  sana watoto.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii anayeshughulikia masuala ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Mathias Haule amesema kuwa mabaraza ya watoto yanatoa fursa kwa watoto kujadili agenda zao na kuwasilisha maoni yao kwenye mamlaka husika ili kuhakikisha kuwa kuzingatia mahitaji ya watoto yanazingatiwa katika mipango, Sera, na maamuzi mbalimbali.  

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa  Shinyanga Bw. Albert Msovela amehaidi kushirikiana na Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii katika kuyalea na kuyapa mwongozo Mabaraza ya watoto ili yaweze kuleta tija katika makuzi ya watoto na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Pia  Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Mkoa wa Shinyanga Victoria Chacha ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali watoto na kuwapatia haki zao hasa haki ya kuendelezwa na kupata elimu ambayo kwa sasa inatolewa bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne.

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amefanya ziara mkoani Shinyanga kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *