Uchumi Zone

Elimu bora kuiwezesha Tanzania kupiga Hatua ya Uchumi wa Viwanda

on

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa uwekezaji katika elimu bora kwa vijana wa kike na wa kiume kutaiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati wa viwanda hata kabla ya mwaka 2025.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo wilayani Kondoa Mkoani Dodoma, wakati wa uzinduzi wa kambi inayowahusisha wanafunzi 260 wa kidato cha pili na cha nne kutoka shule 23 za Sekondari wilayani humo wanaopatiwa mafunzo ya kina  ili kujiandaa na mitihani yao.

Kambi hiyo inafanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo ambapo kiasi cha shilingi milioni 90 za mfuko wa Jimbo la Kondoa zimetumika na kuiwezesha wilaya hiyo kupanda daraja kielimu kutoka nafasi za mwisho kitaifa hadi kufikia nafasi za juu kabisa.

“Athari chanya ambayo ninataka kuiacha Kondoa ni elimu bora kwa vijana wetu inayokwenda sambamba na uamuzi wa Mhe. Rais wetu Dkt. John Magufuli, wa kutoa elimu ya msingi na Sekondari bure kwa wanafunzi hivyo kuongeza thamani ya uamuzi huo wa Serikali,” alisema Dkt. Kijaji

Alisema kuwa baada ya hatua ya Halmashauri ya wilaya hiyo kutoa mtihani wa aina moja wa majaribio kwa shule za msingi na kuonesha mafanikio makubwa, hatua hiyo sasa itaelekezwa kwenye elimu ya Sekondari ili kuwapima vyema wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao ya kitaifa.

Akizungumza kabla ya kuzindua kambi hiyo ya siku 25, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, amesema kuwa taifa lenye wasomi waliobobea katika nyanja mbalimbali wataisaidia nchi kukabiliana na mikataba mibovu inayo pora rasilimali za nchi.

Aliwataka wanafunzi hao kutumia vizuri fursa waliyoipata kwa kusoma kwa bidii na maarifa ili waje kulitumikia taifa ili liweze kufikia maendeleo ya haraka kwa kuhakikisha kuwa wanalinda kwa nguvu zao zote rasilimali hizo za Taifa yakiwemo madini, gesi na mazingira.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Sezaria Makota, amempongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Dkt. Ashatu Kijaji, kwa kusimamia kidete suala la elimu ya watoto wa wilaya yake kupitia mfuko wa jimbo, hatua iliyoifanya wilaya hiyo kupata tuzo mbalimbali za ubora wa elimu katika kipindi cha miaka mitatu.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *