Makala

Hongereni Kidato cha Nne Mliofaulu Lakini Tujitafakari kwa Udanganyifu Huu

on

Tayari matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2017 yameshatangazwa ambapo ufaulu unaonyesha kupanda kwa asilimia 7 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2016. Nichukue fursa hii kuwapongeza wahitimu wote wa kidato cha nne waliofanya vizuri. Na kuwapa pole wahitimu ambao matokeo yamekuwa kinyume na malengo yao.

Naamini wapo ambao kwa namna moja ama nyingine matokeo haya yamewakatisha tamaa, lakini jipeni moyo bado kuna nafasi ya kufanya vizuri katika maisha. Kikubwa kwa sasa tafuteni ushauri bora na wenye kuwajenga maana ukifuata kila shauri lazima maisha yako yawe taabuni.

Nichukue fursa hii pia kuwapongeza wazazi, walezi na walimu pamoja na serikali kwa jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa wanafunzi katika shule wanasoma pasipo kuwa na shida. Japo matatizo hayaishi lakini kwa kiasi chake mmefanya kwa kiasi chenu.

Pamoja na changamoto zote zilizopo lakini serikali imeweka msisitizo wake kuwa elimu ni bure kwa shule za msingi hadi kidato cha nne hivyo wanafunzi wanaosoma katika shule za serikali hawana kisingizio tena cha kushindwa kusoma kwa sababu ya kukosa ada.

Kwa upande wa wazazi na walezi mmepigana vita kuu kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuhakikisha kuwa watoto wenu wanasoma. Wengine mliingia mikopo na wengine kujikuta katika matatizo makubwa ya kudhihakiwa lakini yote hayo mlihakikisha watoto wenu wanasoma hasa wale mliowapeleka katika shule za kibinafsi.

Pamoja na pongezi hizo za dhati kabisa ambazo halikuwa lengo la kuandika makala hii bali utangulizi tu wa kukuvuta msomaji wa ukurasa huu kuja kwenye lengo la makala hii ambalo ni kuhusiana na udanganyifu wa kutisha uliobainika katika mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2017.

Mwishoni mwa mwezi Januari 2018, Baraza la mitihani la Tanzania (NECTA) lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2017mtihani ulifanyika mwishoni mwa mwezi wa oktoba hadi kati ya Novemba 2017.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es salaam Katibu wa Baraza la Mitihani la Tanzania Dkt. Charles Msonge alikaririwa akisema kuwa udanganyifu uliofanyika kwa mwaka 2017 ni wa aina yake ambapo kwa baadhi ya vituo vilibainika wazi kuwa na majibu ya kukosa yenye ufanano.

Katika uwasilishaji wa matokeo hayo Dkt. Msonge aliviambia vyombo vya habari kuwa jumla ya watahiniwa 265 walibainika kufanya udanganyifu wakati wa mitihani hiyo. Ambapo watahiniwa 123 walikamatwa kwenye vyumba vya mtihani wakiwa na vitu visivyoruhusiwa kwenye chumba cha mtihani wakiwa na simu, vitabu na baadhi ya maandiko.

Watahiniwa 62 walikamatwa kwa wakiwa wanabadilishana majibu kwa njia ya karatasi na wengine kuabadilishana namba za mtihani na wengine kuwa na miandiko tofauti kwenye karatasi moja ya kujibia mtihani huo.

Watahiniwa wengine 73 walibainika kuwa na majibu ya kukosa yenye mfanano usio wa kawaida, ambapo katibu wa baraza la mitihani alibaisha kuwa makosa haya yalitokea katika kituo cha Manyovu na Seuta kilichopo Tanga ambapo watainiwa waliandika jibu ambalo halipo kwenye karatasi ya mtihani.

Dkt. Msonge alisema “Katika kituo hicho kwenye mtihani wa Biolojia swali la pili lililowataka watainiwa kuoanisha dhana kati yak undo A na kundi B ambalo lilikuwa na herufi kuanzia A hadi O ambapo watahiniwa katika shule hiyo waliandika P ambayo haikuwepo kwenye orodha ya majibu.  Ambapo kwa kituo hicho hali hiyo ilibainika ni kwa masomo karibu yote ya mtihani huo”

Dkt. Msonge anaonyeshwa kushangazwa na watahimiwa ambao kwa mwaka jana walianzisha jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Tanzania  ambapo alikitaja kituo cha Mwalasi kilichokuwa na watahiniwa 27 wote wa namna hii. Ambao baada ya kukamatwa hawakurudi tena kwenye mtihani hadi mitihani ilipokwisha.

 “Watu wanapanga utaratibu wa kuwafanyia watu wengine lakini wote wanajiandikisha, nao wanakwenda kufanya mtihani huku kila mtu akiandika namba tofauti na aliyosajiliwa ambapo anayefanyiwa mtihani anaandika namba ya anayemfanyia mtihani ambaye anakuwa na uwezo zaidi ili tu afaulu jambo ambalo ni udanganyifu mkubwa” alisema Dkt. Msonge

Mbali na hao wapo pia watuhumiwa 7 waliofanikiwa kukamatwa wakiwa wanawafanyia watu wengine mtihani ambao kwa namna moja ama nyingine ni ndugu au rafiki zao ili tu wafanye vizuri katika mtihani huo.

Tusipokuwa makini na kukuemea vikali udanganyifu huu kwenye mitihani hatutakuwa na maana katika jamii, hawa watahiniwa 265 waliokamatwa laity kama wangekuwa wakweli na waaminifu huenda wangefanya vizuri mitihani nayo na baadaye kuja kulisaidia taifa.

Chonde chonde tunapaswa kujenga jamii ya watu waadilifu ambao wataisaidia serikali na jamii kw ujumla na si kujenga na kuendelea kuchekelea jamii ya watu wadanganyifu na wasioaminika hata kwa vitu vidogo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901, 0716216249 au barua pepe ya barakangofira@gmail.com

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *