Habari Kitaifa

Hali ya Usalama kuelekea Mwisho wa Mwaka yatolewa

on

Jeshi la Polisi Nchini limetoa hali ya usalama wa nchi kwa ujumla kuwa ni ya kuridhisha sana, na takwimu zimeonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba, 2016 makosa makubwa ya Jinai yaliyoripotiwa yalikuwa ni 68,204 ikilinganishwa na makosa 61,794 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2017, ikiwa ni upungufu ya makosa 6,410 ambayo ni sawa na asilimia 9.4.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai CP Robert Boaz ameeleza kuwa makosa dhidi ya binadamu ambayo yanajumuisha makosa ya mauaji, kubaka, kulawiti, wizi wa watoto, kutupa watoto, kunajisi pamoja na usafirishaji binadamu yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2016, yalikuwa 11,513 ukilinganisha na makosa 11,620 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2017 ambayo ni ongezeko la makosa 107 sawa na asilimia 0.9.

Aidha DCI Boaz ameongeza kuwa katika makosa ambayo yameonekana kuongezeka ni makosa ya kubaka na kunajisi ambapo kwa mwaka 2016 hadi kufikia Novemba makosa ya kubaka yaliyoripotiwa yalikuwa 6,985 ikilinganishwa na makosa 7,460 ambayo yameripotiwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la makosa 478 sawa na asilimia 6.8 wakati makosa ya kunajisi yalikuwa 16 kwa mwaka 2016 ikilinganishwa na makosa 25 mwaka huu 2017 na kufanya ongezeko la makosa 9 sawa na asilimia 56.3.

“Makosa dhidi maadili ya jamii ambayo yanajumuisha makosa kama kupatikana na silaha, dawa za kulevya, bangi,  mashamba ya bangi, mirungi, nyara za serikali, magendo, rushwa, uvuvi haramu, kupatikana na mazao ya bahari pamoja na wahamiaji haramu yaliyoripotiwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba 2016, yalikuwa 20,000  ukilinganisha na makosa 18,971 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2017 ambayo ni pungufu ya makosa 1,029 sawa na asilimia 5.1” alisema DCI Boaz.

Katika kuelekea kipindi cha msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya DCI Boaz ametoa tahadhari  juu ya matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakijitokeza sana katika kipindi hiki cha sikukuu yakiwemo matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa magari, utapeli, mauaji  na vitendo vya ubakaji hali inayochangiwa na watu wachache kutumia fursa ya sikukuu  hizo kutaka kujipatia kipato kwa njia zisizo halali.

Ameongeza kuwa katika msimu huu wa sikukuu hizi wamejipanga vyema kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu vitakavyojitokeza katika kipindi hiki na ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo ambayo  yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *