Habari Kitaifa

Malezi Bora ni Msingi Katika Ujenzi wa Familia Imara na Taifa Imara

on

Malezi bora katika familia imesemeka ni ndio msingi wa malezi kwa watoto katika jamii yetu hivyo wazazi wanapaswa kuzingatia kutoa malezi bora kwa watoto ndani ya familia na jamii kwa ujumla ili kuwa na taifa lenye uchu wa kujiletea maendeleo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe.Vaileth Makota  wakati akisoma Hotuba ya Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika  maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika Wilayani Kondoa katika Mkoa wa Dodoma.

Mhe. Vaileth Makota amesema kuwa wazazi wanawajibu wa kuwalea watoto katika malezi bora na katika maadili mazuri ili kujenga taifa bora lenye watoto wanaojitambua, wanaojithamini, na wenye maadili mema ili kulitumikia Taifa.

Ameongeza kuwa wazazi wanatakiwa kuwa walimu kwa matendo yao kwa watoto kwani watoto wanaiga yale ambayo wazazi wanafanya hivyo tabia na mienendo yao ni kati ya vitu ambavyo vitasababisha malezi mabaya au bora kwa watoto na jamii kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa wazazi wana wajibu wa kuwalea watoto katika malezi bora ili kujenga utu, uzalendo na upendo kwa watoto na jamii kwani malezi katika familia ni msingi katika ujenzi wa taifa linalozingatia uzalendo, maadili mema, utu na uwajibikaji katika maendeleo yao na taifa.

“Tuzingatie katika kutoa malezi bora kwa watoto wetu ili tujenge taifa bora lenye maadili mema kwa maendeleo ya taifa,” alisisitiza Mhe. Vaileth

Kwa  upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mtoto Bi. Magreth Mussai amesisitiza watoto na vijana kuwa na maadili kwa wazazi na wanajamii ili kujenga taifa lenye maadili na upendo.

Siku ya Familia Duniani inaadhimishwa kila Mei 15, 2018 na kwa mwaka huu inaadhimishwa ikienda na kaulimbiu isemayo “Malezi Jumuishi: Msingi wa Uzalendo, Utu na Maadili ya Familia na Taifa,’’.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *