Habari Kitaifa

Mamia wamuaga Mwanahabari Nguli Justine Limonga

on

Katibu  wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamphrey Polepole, ameongoza mamia ya waombolezaji katika ibada ya kuaga mwili wa mwanahabari, Justine Limonga iliyofanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam leo mchana.
 
Akizungumza katika ibada hiyo, Polepole alisema CCM na tasnia ya habari imepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa bado akitegemewa na wamempoteza mtu muhimu ambaye alikuwa akitegemewa kama chama na kuahidi kuangalia namna ya kuisaidia familia ya marehemu aliyoiacha.
Naye Mkurugenzi wa Nduvini Auto Garage, Alhaji Ahmed Msangi alizungumza jinsi alivyomfahamu marehemu ambapo aliahidi kampuni yake kwa kipindi hiki cha kufunguliwa kwa shule itawanunulia vifaa vya shule, sare na kuwalipia karo wakati wakisubiri kukaa na familia kuona namna ya kuwazesha watoto hao kielimu.
Kwa upande  wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uhuru FM, Angel Akilimali alisema kifo cha mwanahabari huyo aliyekuwa mwajiriwa wao kimeacha pengo kubwa ambalo halitazibika.
Alisema Limonga alikuwa mhariri na mbunifu na aliweza kuongoza vipindi mbalimbali ambavyo vilipendwa na wasikilizaji wa Uhuru FM ambapo aliahidi stahiki zote za marehemu kama mwajiriwa zitapatikana kwa wakati.
Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini, siasa wanamuziki na wanahabari na wananchi iligubikwa na majonzi na baadhi ya watu kushindwa kujizuia kulia.
Akitoa mahubiri kwenye ibada hiyo Katekista wa Parokia ya Kutukuka kwa Msalaba Kizuiani, Philo Mbunda alisema mwenzetu Limonga amemaliza kazi ya hapa duniani je sisi tuliobakia tumejiandaeje
Katekista Mbunda alisema kila mtu anapaswa kujitafakari maisha yake ya kiroho kabla ya kifo na hivyo ndivyo Mungu wetu anavyohitaji.
Limonga alifariki dunia Desemba 31, mwaka jana katika Hospitali ya TMJ alipokuwa akitibiwa na ameacha mjane na watoto wawili ambapo mazishi yake yamefanyika leo katika Makaburi ya Saku yaliyopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *