Habari Kitaifa

Polisi DSM: Matukio ya Ki-uhalifu yamepungua Mwaka 2017

on

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es  salaam limetoa taarifa za matukio ya kiuhalifu na usalama  barabarani yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi Kanda maalumu  Dar es salaam katika  kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba 2017.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam SACP Lazaro Mambosasa ameeleza kuwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2017 matukio ya kiuhalifu yaliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi ni 126,200 ukilinganisha na kipindi kama hicho 2016 ambacho kilikuwa na matukio 129,602 hivyo kusababisha upungufu wa matukio  3,405 sawa na asilimia 2.6.

Aidha Kamanda Mambosasa amesema kulikuwa na matukio makubwa ya jinai 9,736 ukilinganisha na matukio makubwa ya jinai 12,550 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2016 na upungufu wa matukio 2,814 sawa na asilimia 22.4 na hali ya uhalifu katika Kanda ya Dar es salaam ilikuwa ya kuridhisha ingawa matukio machache ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji, wizi wa magari pamoja na pikipiki.

“Katika opereshi mbalimbali zilizofanywa na Jeshi la polisi tuliweka juhudi na kuiimarisha usalama wa wananchi na pia kuimarisha doria na misako mbalimbali sehemu zote za jiji ambapo wahalifu wapatao 18,194 walikamatwa kwa tuhuma mbalimbali kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2017” alisema Kamanda Mambosasa.

Pia Jeshi la polisi limeomba kupatiwa ushirikiano kwa wananchi wa jiji la Dar es salaam katika kupunguza uhalifu hasa katika kipindi cha kuelekea shamrashamra za sikukuu ya Mwaka Mpya na Kamanda Mambosasa amepiga marufuku ulipuaji wa fataki mitaani na sehemu ambazo sio rasmi pamoja na uchomaji wa matairi barabarani na kueleza sehemu iliyoruhusiwa ulipuaji wa fataki ni katika viwanja vya Tanganyika Packers na kwenye hoteli zilizopewa vibali na jeshi la polisi kwa kibali maalumu.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *