Uchumi Zone

Mawaziri na Magavana Jumuiya ya Afrika Mashariki Wajadili Kuiwezesha Sekta Binafsi Kukua

on

Sekta binafsi inatakiwa kuhakikisha fedha  inazokopa kwa ajili ya uwekezaji au biashara zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili waweze kurejesha mikopo yao kwa wakati na hivyo kupunguza ongezeko la Mikopo Chechefu (NPL).

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyasema hayo wakati wa mkutano wa uwekezaji uliojumuisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioangazia changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi kutoka taasisi za fedha katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, katika mikutano ya kipupwe inayoendelea mjini Washngton DC, Marekani.

Amesema kuwa, licha ya kuwepo kwa wakopaji wasiorejesha mikopo kwa wakati pia mwenendo mzima wa baadhi ya taasisi za fedha zikiwemo benki kutozingatia kanuni na taratibu za ukopeshaji, jambo linalosababisha kuongezeka kwa mikopo chechefu.

Akizungumzia kuhusu kupungua kwa mikopo kwenye Sekta binafsi katika Jumuiya hiyo, Waziri Mpango amewataka wananchi watambue kuwa ziko changamoto ambazo zinatokana na mahusiano ya kiuchumi ya ulimwengu yanayosababisha kupungua kwa bidhaa ambazo zinauzwa nje  ya nchi hivyo kuathiri sekta binafsi.

Amesema matokeo kupungua kwa biashara ama mauzo nje ya nchi kumewafanya wafanyabiashara kupunguza uwezo wao wa kurejesha mikopo waliyokopa katika benki, hivyo wananchi wasione kama ni tatizo la jumuiya hiyo tu bali lazima kuunganisha kinachotokea na  mwenendo wa kibiashara kimataifa.

Sababu nyingine ni kupungua kwa fedha zilizokuwa zinaingia katika mfumo wa kibajeti miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kutoka kwa nchi wahisani na hivyo kuzifanya nchi kukopa kwenye taasisi za fedha za ndani  ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“ Katika majadiliano haya tumekubaliana kuendelea kuzungumza na sekta binafsi na kushughulikia matatizo  yanayowakumba hasa suala la malipo ya madai yao mbalimbali ili waweze kulipwa haraka na kuondoa vikwazo katika mitaji yao ya biashara ili waweze kurejesha mikopo waliyokopa katika benki.” alisema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga, ambaye alishiriki majadiliano hayo ya uwekezaji alisema kuwa, sekta binafsi ina umuhimu mkubwa katika kukuza maendeleo ya nchi kupitia uwekezaji wao.

“Nchi za Afrika Mashariki zisipokuwa na uwekezaji mkubwa kupitia sekta binafsi, benki zitakosa utayari wa kutoa mikopo kwa sekta hizo kwa kuwa na wasiwasi wa urejeshwaji wa mikopo hiyo,” alieleza Gavana Luoga.

Amesema nchini Tanzania benki  binafsi zimeanza kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta binafsi, hata hivyo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inafanya majadiliano na benki hizo ili kuangalia jinsi zinavyoweza kuongeza uwekezaji kwa kutoa mikopo huku jambo linalotakiwa kutiliwa mkazo ni ushirikiano na sekta hizo ili ziweze kukopesheka suala ambalo Serikali imekuwa ikilijadili pia na nchi nyingine na kuwa na mafanikio chanya.

Mkutano huo wa uwekezaji uliojumuisha nchi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulihudhuliwa na  Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu za Afrika Mashariki na kuwa na mafanikio makubwa kwa mstakabali wa maendeleo ya jumuiya hiyo hasa katika Sekta ya Fedha.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *