Habari Kitaifa

Naibu Waziri Nishati Aikaribisha Kampuni ya Italia Kuzalisha Umeme Nchini

on

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu ameikaribisha kampuni ya kimataifa ya kuzalisha umeme kutoka nchini Italia ijulikanayo kama Ansaldo Energia kuwekeza katika Sekta ya Nishati hususan uzalishaji umeme kwa kutumia Joto Ardhi.

Naibu Waziri ameyasema hayo katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kati yake na Balozi wa Italia aliyefika ili kuitambulisha kampuni hiyo inayojishughulisha na uzalishaji wa umeme katika nchi mbalimbali duniani.

Akizungumza katika kikao hicho Mgalu amesema kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania inatarajiwa kuingia katika uchumi wa kati na ili kuiwezesha kufikia uchumi huo Serikali imedhamiria kujikita katika uchumi wa Viwanda ambao kwa kiasi kikubwa unategemea nishati ya umeme.

“ Ili kuweza kuendesha uchumi wa Viwanda nchini, Serikali inakaribisha kampuni binafsi kuzalisha umeme na hivyo kuongeza kiasi cha umeme kitakachokidhi mahitaji ya nchi,” alisema Mhe. Mgalu.

Ameongeza kuwa, Tanzania ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na Maji, Gesi, Upepo, JotoArdhi na Makaa ya Mawe, hivyo alimweleza Afisa Mauzo wa Kampuni ya Ansaldo, Stefano Boggia kufanya utafiti ili kujua wanataka kuwekeza kwenye eneo gani kisha wawasilishe maombi rasmi wizarani ili kuendelea na hatua zinazofuata.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni amesema kazi yake kama Balozi ni kupokea maombi ya wawekezaji kutoka Italia wenye nia ya kuwekeza nchini na kuwatambulisha kwa Serikali ili kuendelea na hatua za uwekezaji.

Aidha, ameiomba Serikali kuainisha maeneo ya vipaumbele katika Sekta ya Nishati na kuviwasilisha ubalozini ili iwe rahisi kwao kuyaelekeza makampuni yenye nia ya kuwekeza nchini.

Akielezea uzoefu wa kampuni hiyo, Afisa Mauzo wa Kampuni ya Ansaldo, Stefano Boggia amesema kuwa kampuni hiyo imejenga mitambo miwili ya kuzalisha umeme nchini Afrika Kusini, pia wana mitambo ya umeme nchini Italia na nchi za Ulaya ambapo katika maeneo yote wanazalisha kiasi cha megawati 16,000.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga ameahidi kuainisha miradi ya umeme inayohitaji uwekezaji na kuwasilisha Ubalozi wa Italia nchini pamoja na kwa Afisa Mauzo wa kampuni ya Ansaldo ili waweze kutumia kama mwongozo wa kufanya maamuzi ya eneo watakalopenda kuwekeza.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *