Habari Kitaifa

NEC yatangaza tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Marudio katika Majimbo ya Siha na Kinondoni

on

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa uchaguzi mdogo katika majimbo ya Siha mkoani  Kilimanjaro na Kinondoni mkoani  Dar es Salaam pamoja na Kata nne za Tanzania Bara utafanyika Februari 17, 2018 kufutia waliokuwa Wabunge katika majimbo hayo kujivua Uanachama na kukosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmod Hamid imeeleza kuwa pamoja na Majimbo hayo, pia Kata nne za Isamilo katika  Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Manzase Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Madanga Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga na Kimagai  Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma zitafanya Uchaguzi mdogo.

Aidha, Jaji  Mkuu Mstaaafu Hamid  amesema  kuwa, Tume inaendesha uchaguzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mh. Job Ndugai kuhusu uwepo wazi wa jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.

Jaji Mahmoud amesema kuwa, barua hiyo ilieleza kuwa majimbo hayo yapo wazi baada Maulid Mtulia aliyekuwa Mbunge  wa Jimbo  la  Kinondoni  kujivua  uanachama  wa  CUF  na  Dr.  Godwin  Mollel  wa  jimbo  la  Siha  kujiuzulu  uanachama  wa  CHADEMA  na  hivyo  wote  kukosa  sifa  za  kuwa  Wabunge.

Pia,  ameeleza kuwa Tume  ilipokea  taarifa  kutoka  kwa  Waziri  mwenye  dhamana  ya  Serikali  za  Mitaa  ikiitaarifu  Tume   uwepo  wa  nafasi  wazi  za  Udiwani katika  kata  nne  za  Tanzania  Bara.

“Baada  ya  kupokea  barua  hizo  Tume  kwa  kuzingatia  vifungu  vya  37(1)  na  46(2)  vya  Sheria  ya  Taifa  ya  Uchaguzi  sura  ya  343  pamoja  na  kifungu  cha  13(3)  cha  Sheria  ya  Uchaguzi  wa  Serikali  za  Mitaa  sura  ya  292  inatangaza  kuwa  majimbo  mawili  na  kata  nne  zipo  wazi”  alisema  Jaji  Mahmoud.

Ameeleza  kuwa, fomu  za  uteuzi  kwa  majimbo  hayo  mawili  na  kata  nne  itakuwa  kati  ya  tarehe  14  – 20  Januari,  2018,  uteuzi  wa  wagombea  utafanyika  tarehe  20/01/2018, na Kampeni  za  uchaguzi  mdogo  zitafanyika  kuanzia  tarehe  21/01 – 16/02/2018  na  siku  ya  uchaguzi  itakuwa  tarehe  17/02/2017.

Vilevile,  Jaji  Mahmoud  amevikumbusha  Vyama  vya  Siasa  na  wadau  wote  wa  uchaguzi  kuzingatia  sheria,  kanuni,  taratibu,  miongozo  na  maelekezo  yote  wakati  wa  uchaguzi  huo  mdogo.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *