Habari Kitaifa

Rais MAGUFULI: Baadhi ya Ninaowateua hawajui Ninachokitaka

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 08 Januari, 2018 amemuapisha Mhe. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini na kuiagiza Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kanuni za sheria mpya ya madini namba 7 ya mwaka 2017 inasainiwa ifikapo Ijumaa tarehe 12 Januari, 2018.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya Mhe. Biteko kuapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na ameelezea kutoridhishwa kwake na namna viongozi na watendaji wa Wizara ya Madini wanavyotekeleza majukumu yao polepole na bila kujali maslahi ya nchi.

“Sheria hii imepitishwa na Bunge na mimi nikaisaini tangu mwezi wa 7 mwaka 2017, mpaka leo ni miezi 7 bado hamjasaini kanuni zake ili sheria ianze kutekelezwa, na wahusika wote wapo, yaani mpaka leo hamjaelewa Watanzania wanataka nini? amesema Mhe. Rais Magufuli.

Amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi kushirikiana na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wanaohusika katika Wizara ya Madini kuhakikisha kanuni hizo zinasainiwa.

Wakati huo huo….

Naibu Waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko ambaye ameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Madini tarehe 8 Januari, 2018 ameanza kazi rasmi kwa kufanya kikao na Viongozi na  Watumishi wa Wizara husika.

Kikao hicho kimefanyika  katika ukumbi wa Wizara jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu, Profesa Simon Msanjila.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu  Waziri huyo alieleza kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya viongozi na watumishi wa Wizara ili kwa pamoja wasimamie ipasavyo Rasilimali Madini na kuhakikisha kuwa inafaidisha Taifa.

“ Ili kutimiza malengo ya Rais wetu ya kuhakikisha kuwa Rasimali Madini inaendelezwa ipasavyo,  hatuna budi kushirikiana na kushikamana  ili kuwe na umoja utakaoleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwani sisi sote ni watumishi wa watanzania,” alisema Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Uteuzi wa Naibu Waziri wa Pili katika Wizara ya Madini unaonesha namna Rais John Magufuli anavyoichukulia kwa umuhimu wa pekee Sekta ya Madini ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

“ Tutashirikiana kwa pamoja na watumishi wa Wizara ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele zaidi,” alisema Nyongo.

 

About Habari360_1

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *