Habari Kitaifa

RC Makonda Afurahishwa na Waliokubali Kutunza Watoto

on

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameongeza siku tano zoezi la kuwapatia msaada wa kisheria wakina mama waliotelekezwa na waume zao,ambapo amesema kwanzia wiki ijayo wataanza kusikilizwa wakina baba wanaolalamikiwa pamoja na kuwasikiliza wakina mama waliobakia na kuwataka wanaume watakaoitwa wafike bila kukosa ili kuepusha kutajwa majina yao hadharani.

Akizungumza na akinamama waliofurika ofisini kwake leo, Mhe. Makonda ameeleza kuwa wanaume watakaopewa wito wa kufika ofisini kwake na kukaidi agizo la kufika hapo jina lake litatajwa hadharani na kuwapongeza akina baba waliokubali wito wa kufika na kusema kuwa kuanzia wiki ijayo wakina baba wanaolalamikiwa wataanza kufika kwa ajili ya upatanishi.

“Wakina baba wanaolalamikiwa waliopewa wito wataanza kufika kuanzia jumatatu wiki ijayo kwa ajili ya upatanishi na wale watakaokaidi tutataja majina yao hadharani hivyo wakina baba watakaokaidi kuja kwa ajili ya kupatanishwa nitawatangaza  majina yao hadharani na nyie mlioko nyumbani mna haki ya kubeza hili zoezi na haki ya kuandika mnachoandika lakini mimi namtazama mama anayeteseka, kwa hiyo waache waseme wanachokisema lakini mimi furaha yangu ni amani ya watoto na kina mama wanaoteseka” alieleza Bw. Makonda.

Aidha ameongeza kuwa zoezi hilo lina faida kwa wakinamama wote hata walioko kwenye ndoa kwani litasaidia kuwapatia haki watoto wote na kusaidia watoto kufahamika katika familiya na kubainisha kuwa hii itasaidia kupunguza wakina dada wanaowaza kutoa mimba ama kutupa watoto wachanga na kuwaasa wakina mama na wanawake wote wa mkoa huo kutumia kinga wakati wanapofanya tendo la ndoa ili kupunguza kasi ya Ugonjwa wa UKIMWI kwani kwa kipindi kifupi ugonjwa huo umeongezeka kwa asilimia 45% kwa watoto wenye umri chini ya miaka 24.

“Tunataka katika mkoa huu kina dada wasiwaze kutoa mimba, wasiwaze kutupa kichanga na wanaume wanaopanga kuwapa mimba mwanamke kama ajajipanga aogope kama ilivyo kubaka”Aliongeza Bw. Makonda

Tangu kuanzishwa kwa zoezi la usikilizwaji wa akina mama waliotelekezwa na kupatiwa msaada wa kisheria zaidi ya kina mama 10,000 wamefika kupata huduma na kati yao wanawake 400  wamesikilizwa na familia 205, wamekubali kwa maandishi kuwahudumia watoto wao na wengine 21 wamepimwa DNA.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *