Uchumi Zone

Serikali Yajipanga Kuwajengea Uwezo Watoa Huduma Katika Sekta ya Utalii

on

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewasilisha  rasimu ya   kanuni ya kusimamia watoa huduma katika sekta ya utalii na ukarimu kwa wadau wa sekta hiyo  ili waweze kutoa maoni yao  yatakayosaidia katika kuboresha kanuni hizo ili ziweze kuwasimamia wafanyakazi  kwa kuhakikisha kuwa  huduma zinazotolewa   zinazokidhi viwango vya kimataifa kwa watalii.

Akizungumza mjini Dodoma kwenye  mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta hiyo  kwa ajili ya kupitia Rasimu ya kanuni hiyo,  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki alisema Wizara imeandaa rasimu hiyo  ili kutoa nafasi kwa wadau  kuipitia na kutoa maoni yatakayoisaidia katika kuiboresha.

Akizungumzia moja ya  lengo la kanuni hizo ni  kutaka  kuwajengea uwezo wafanyakazi wa tasnia hiyo ili waweza kushindana katika soko la ajira la kitaifa na kimataifa.

Aliongeza kuwa kanuni hizo  pia  zitasaidia  kuwawekea ulinzi na usalama katika taaluma hiyo pamoja na kuleta uwajibikaji na uaminifu katika kutoa huduma kwa vile kutakuwa na  mfumo wa kuwatambua.

Alisema hatua hiyo ya ukusanyaji maoni  imekuja baada ya sekta hiyo ya  kukabiliwa na changamoto ya huduma hafifu zinazotolewa kwa watalii hususani wale wa kimataifa.

Alisema hali hiyo imechangiwa na ukosefu wa chombo cha kusimamia viwango vya huduma zinazotolewa katika sekta hiyo.

Alisema kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka watalii kuwa huduma wanazopata ni hafifu.

Awali, Mkurugenzi wa idara ya Utalii, Deograsias Mdamu, alisema majadiliano hayo  ya kuboresha  kanuni hizo yatasaidia kuwa na wafanyakazi mahiri na wenye weledi katika tasnia hiyo.

Aliongeza kuwa,  maoni hayo yatapelekea kuunda kanuni bora na shirikishi zitakazosaidia  katika kuwasimamia wafanyakazi na waajiri  katika kutoa huduma  bora kwa watalii kwa kila mmoja kwa nafasi yake.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha waongoza watalii Tanzania, Emannuel Mollell aliipongeza Wizara kwa hatua h iliyofikia ya kuandaa rasimu hiyo kwa vile rasimu hiyo  inatoa muelekeo mzuri  katika sekta ya utalii na ukarimu nchini.

Akichangia maoni Katibu huyo , Emanuel Molleli alisema ni vyema  kanuni  igusie maslahi ya wafanyakazi    kwani hicho kimekuwa  ni kilio chao cha  muda mrefu lakini katika  rasimu hiyo hakuna kipengele chochote kilichozungmzia suala hilo.

Aliongeza kuwa  wafanyakazi wa tasnia hiyo kwa ujumla wake  wamekuwa wakilipwa mshahara midogo sana hali inayoplekea kushusha morali katika kuwahudumia watalii kwa viwango bora.

 Kutokana na uwasilishwaji wa maoni hayo , hali hiyo ilimfanya   Mkurugenzi wa Idara ya hiyo, Mdamu kumjibu    kuwa suala hilo litaangaliwa.

Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Bety Begashe wakati akichangia maoni aliiomba  Wizara iiangalie namna bora itakayosaidia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi hao mbali na mitihani itakayokuwa inafanywa na wanatasnia hao.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *