Habari Kitaifa

TAKWIMU: Maambukizi ya Ukimwi yapungua Hadi Asilimia 4.7

on

KIWANGO cha maambukizi ya UKIMWI nchini kimepungua kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2016/2017.

Akizindua matokeo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa Mwaka 2016/2017, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na janga la UKIMWI.

Amesema kwa mujibu wa utafiti huu wa mwaka 2016/17, inakadiriwa kuwa watanzania wapatao million 1.4 wanaishi na virusi vya UKIMWI. Alifafanua kuwa utafiti huo unaonesha kuwa kiwango cha maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.5 na wanaume ni asilimia 3.5.

Mh. Samia Suluhu amesisitiza kuwa kupungua kwa kiwango cha maambukizi hakumaniishi kuwa UKIMWI umeisha bali ni matokeo ya jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo wananchi katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.

“Utafiti huu tunaouzindua leo umeonyesha kupungua kwa kasi ya maambukizi ya UKIMWI kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 4.7 kwa mwaka 2016/2017. Hii inatokana na juhudi za pamoja kati ya Serikali, wananchi na wadau mbalimbali waliojikita katika kutoa elimu na huduma za masuala ya UKIMWI,” amesema Mh. Samia Suluhu.

Mh. Samia Suluhu ametoa wito kwa wananchi na wadau wengine kuendelea kuiunga mkono Serikali katika kukabiliana na maambukizi mapya pamoja na kuchangia kwa hiari Mfuko wa Taifa wa UKIMWI ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora zinazohusu UKIMWI.

Mapema akitoa maelezo kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa huo ni utafiti wa nne kufanyika hapa nchini, ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2003/04 ambao ulionesha kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 7.0  na kufuatiwa na tafiti nyingine za miaka ya 2007/08 na 2011/12 iliyoonesha maabukizi ya asilimia 5.1.

Alieleza kuwa utafiti wa 2016/17 umekuwa wa kipekee kwani unatoa makadirio ya kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote  ikiwa ni pamoja na maambukizi mapya ya VVU, kiasi cha VVU mwilini kwa wanaoishi na VVU, na kiwango cha kufubazwa kwa VVU mwilini kwa wanaotumia dawa za kufubaza VVU.

Aidha, utafiti huo unatoa kiwango cha maambukizi ya Homa ya Ini  na taarifa za upatikanaji wa huduma na matibabu kwa wanaoishi na VVU pamoja na ushauri nasaha, upimaji wa VVU na utoaji wa majibu, na kukusanya taarifa za kaya na taarifa binafsi za wanakaya.

Amesema utafiti huu ulihusisha kaya 16,198 na kujumuisha wanakaya wote waliokuwa kwenye kaya wakilishi zilizochaguliwa na umegharimu kiasi cha Shillingi 7.4 bilioni ambazo zimetolewa na Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais
wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI (President’s Emergency Plan for AIDS Relief – PEPFAR).

Aidha, amesema mikoa ambayo kiwango cha maambukizi ya VVU ni zaidi ya asilimia 10 ni Iringa yenye maambukizi ya asilimia 11.3 na Njombe yenye asilimia 11.4 huku mikoa yote ya Tanzania Zanzibar ikiwa na maambukizi ya ukimwi ni chini ya asilimia 1.

Katika maelezo yake hayo, Dkt. Chuwa ameonya baadhi ya watu wanaopotosha takwimu rasmi za serikali na kueleza kuwa jambo hilo halikubaliki.

Alibainisha kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu haimzuii mtu kufanya tafiti kwani serikali inatambua kuwa tafiiti ni suala muhimu lakini katika kufanya hivyo lazima mtafiti afuate taratibu zilizowekwa.

Ametoa wito kwa serikali hususani wizara ya afya kutumia matokeo ya utafiti yaliyozindualiwa katika kupanga mipango ya sekta ya afya.

About Habari360_1

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *