Habari Kitaifa

TAMISEMI PS3 Wapongezwa kwa Mifumo

on

Washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Epicor 10.2 katika kituo cha Mwanza, wamepongeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma PS3 kwa jitihada madhubuti wanazochukua katika kuimarisha mifumo ya Sekta ya umma ukiwepo mfumo wa Epicor 10.2.

Wakiongea kwa Nyakati tofauti wakati wa mahojiano maalum, na Mwandishi wetu, Wahasibu na Wekahazina kutoka mikoa ya Mwanza, Tabora, Simiyu, Geita, Kagera na Mara, wemesema katika kuimarisha mifumo mbali mbali ya Sekta ya umma toka mradi wa PS3 umeanza umejitahidi sana kuimarisha mifumo.

Hussein Yahaya  Mhasibu kutoka Halmashauri ya Tabora, amesema katika kipindi kifupi ambacho wameanza kutumia mifumo mbalimbali ikiwepo mfumo wa Epicor  ambao ulikuwa na matoleo yaliyo tangulia, tija na ufanisi umeongezeka tofauti na wakati wa kipindi cha nyuma.

“Ofisi ya Rais ya TAMISEMI imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mifumo inaimarika ukiacha mfumo huu wa kihasibu wa mapato na matumizi Epicor 10.2  ambao  tumejifunza kwa sasa, lakini vilevile katika maeneo yetu kuna mifumo mingine ambayo tunaifanyia kazi kama vile Mfumo wa ukusanyaji mapato katika Halmashauri (LGRCIS), Mfumo wa Hospitali wa mapato pamoja na utabibu (GoTHoMIS), mfumo wa mipango na mbajeti (PlanReP)  na mingine tunayoifanyia kazi yote imetokana na jitihada za Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na mradi wa PS3, anasimulia Hussein.

Maafisa hao ambao walikuwa katika Semina wakijifunza mfumo wa EPICOR 10.2 mkoani Mwanza, wamesema kuwa, Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma PS3 toka umeanza kufanya kazi katika maeneo yao umekuwa chachu ya mabadiliko hasa katika suala zima la mifumo.

“Ukiangalia mradi huu upo katika mikoa 13 na Halmashauri 93 nchini, mkoa wetu wa Tabora haupo katika mradi, lakini kwa jitihada za pekee za Wizara kupitia idara ya TEHAMA wizarani wamekuwa wakihakikisha hata sisi mikoa ambayo siyo ya mradi inajumuishwa katika mabadiliko yote ya msingi na mfano mzuri ni mfumo huu wa Epicor 10.2 ambao umeboreshwa na sasa watendaji kutoka Halmashuri zote 185 zinapatiwa mafunzo chini ya udhamini wa mradi wa PS3.

Mbali na kutoa pongezi kwa Wizara OR-TAMISEMI na mradi wa PS3 wataalam hao hawakuacha kutoa maoni yao kuhusu mfumo wa Epicor 10.2 kuhusu uzuri wa mfumo kwamba mfuo huo ni mzuri na utasaidia sana katika kuimarisha utendaji wao.

Deusderit Binamungu, Afisa Manunuzi kutoka Halmashauri ya Musoma, alisema, mfumo wa Epicor10.2 ambao kwa sasa utaanza kutumika kuanzia mwezi 01 Julai, 2018 ni mfumo wenye kasi lakini unaowezesha kupatikana kwa taarifa kwa muda muafaka.

“Kupitia mfumo wa Epicor 10.2, udhibiti wa masuala ya msingi utaimarika, kabla ya Epicor 10.2 suala la masurufu lilisumbua katika urejeshwaji wake, sheria ya manunuzi namba 7 ya 2011 na marekebisho yake ya 2016, inataka ndani ya siku 14 mtu aliyechukua masurufu awe amefanya maresho toka siku aliyo maliza kazi, lakini ilikuwa tofauti. Hivyo kuanza kutumika kwa mfumo itasaidia kwakuwa Mfumo utakapo anza kutumika mtumishi hataruhusiwa kuchukua masurufu mapya kabla yakufanya maresho ya awali kwakuwa  mfumo utagoma,” amesema Binamungu.

Rozalina Tarimo Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi kutoka Halmashauri ya Maswa, alisema Mfumo wa Epicor 10.2, ni mzuri kwakuwa suala la watumiaji wa mfumo kila mtumiaji atakuwa na namba maalum ya siri hali itakayosaidia kuongeza zaidi usalama lakini pia idadi ya watumiaji kulingana na majukumu yao.

“Kuongezaka kwa mambo haya ya msingi kutaongeza uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja katika nafasi yake na kuondoa utendaji wa kutegeana kwa baadhi ya watendaji wazembe” alisema Rozalina.

Mfumo wa Epicor 10.2 ni mfumo uliosanifiwa na wataalam wa ndani na umekuwa na maboresho ya mara kwa mara ambayo yamesaidia kuongeza tija na ufanisi katika suala zima la utendaji wa shughuli za serikali.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *