Habari Kitaifa

TANESCO yaagizwa kuwaunganishia Umeme Wateja Waliokwisha Lipa

on

Serikali imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha wateja wote walioomba na kulipia huduma hiyo mwaka 2017 wanaunganishiwa kabla ya Desemba 30 mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Singida na Dodoma.

“Agizo hili ni kwa nchi nzima. Hakikisheni wateja waliowasilisha maombi yao na kulipia ndani ya mwaka huu wa 2017 wawe wameunganishiwa umeme siyo zaidi ya Desemba 30 mwaka huu.”

Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa shirika hilo kutoa elimu kwa umma, hasa wananchi walioko vijijini kuhusu umuhimu wa kutumia umeme ili kuwahamasisha kuunganisha nishati hiyo katika makazi yao.

Akifafanua, Waziri alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawajaunganisha umeme katika makazi yao japokuwa tayari Serikali imekwishawafikishia nishati hiyo katika maeneo yao.

“Inawezekana baadhi ya wananchi hawajatambua umuhimu wa kutumia umeme, hivyo ni vema wapatiwe elimu husika. Tuwatembelee mahali waliko, hususan vijijini na tuwapatie elimu hiyo,” alisisitiza.

Akizungumzia faida za umeme, Waziri Kalemani alisema umeme ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinahitaji nishati hiyo.

Aliongeza kuwa, ili dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda ifanikiwe, ni lazima kuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika. “Ndiyo maana tumedhamiria kufikisha umeme hadi vijjijini kwa kasi kubwa, hivyo wananchi tafadhali tumieni umeme ili kukuza pato lenu na uchumi wa nchi kwa ujumla.”

Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani jimboni kwake hivi karibuni, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto), akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, jimboni kwake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akiwakabidhi baadhi ya wazee kifaa kinachotumika kuunganisha umeme pasipo kutandaza mfumo wa nyaya, kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) alipokuwa katika ziara ya kazi Mikoa ya Singida na Dodoma hivi karibuni.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Idifu, Wilaya ya Chamwino alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

About Habari360_1

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *