Habari Kitaifa

Tanzania Kufaidika na Mradi Maendeleo ya Kijamii Kutoka Korea Kusini

on

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inategemea kunufaika na mradi maalum kutoka Shirika la ‘International Youth Fellowship’ lenye makazi yake nchini Korea ya Kusini kuhusu utoaji wa mafunzo ya kuiwezesha jamii kuwa na tabia, fikra na mtazamo chanya ili kuwa na ari na hamasa ya kufikia mabadiliko ya kweli na endelevu katika kujiletea maendeleo ya jamii yenyewe na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika Kikao kati ya Serikali na Shirika hilo Katibu Mkuu Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga amesema  kuwa Mradi huu ni muhimu sana katika jamii ya watanzania kwani utasaidia kubadilisha fikra za watanzania katika kukuza ari na raghba ya kujiletea maendeleo wenyewe katika maeneno yao.

Bi. Sihaba ameongeza kuwa elimu hii itasaidia kuimarisha fikra chanya kwa watanzania wote kujitambua na kuona kuwa maendeleo ya kweli na endelevu yanatokana na ufahamu, uelewa na utashi wa wananachi waliojitoa kufanya kazi za maendeleo kwa kushirikiana na Serikali yenyewe ili kutatua changamoto zilizopo na hivyo  kujifikia maendeleo jumuishi kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Aidha, akizungumza wakati akitoa elimu hiyo kwa ujumbe wa Menejimenti ya Idara kuu Maendeleo ya Jamii, Katibu Mkuu wa Shirika la ‘International Youth Fellowship’ Dkt. Hun Mok Lee amesema kuwa mabadiliko ya fikra ni muhimu katika mendeleo ya Taifa lolote na kama Tanzania inataka kuendelea zaidi inabidi ianze kutoa elimu itakayosaidia kuwajenga na kubadili fikra za watoto na vijana kuhusu utashi wao wa kutatua vikwazo na changamoto ili kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Dkt. Lee ameongeza kuwa ili kuwa na taifa imara zaidi Serikali haina budi kuwarithisha wananchi elimu itakayowawezesha kuwa tayari wa kubadili mtindo wa maisha yao kwa kuwa na mtazamo mmoja wa kushirikiana pamoja katika  kila jambo ili kuchangia azma ya kufikia maendeleo thabiti ya watu na Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amesema kuwa Mradi huu unaendana kabisa na dhana ya maendeleo ya jamii na utasaidia kuongeza chachu katika kuleta mabadiliko ya fikra za wananchi kuweza kujitoa kwa dhati kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kuhakikisha kuwa maisha ya watanzania yanashamiri na uchumi wa Taifa unapaa. 

Katika kutekeleza mpango huu, Wataalam wa Maendeleo ya jamii wataendelea kuraghibisha jamii kubadili tabia zao kutoka katika desturi za uchumi wa vijungu jiko na imani hasi na hivyo kuwa na fikra chanya zinazochochea azma ya kujiletea maendeleo.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *