Uchumi Zone

TBL kujenga Kiwanda kikubwa cha Bia mkoani Dodoma

on

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia TBL, Bw. Roberto Jarrin ambaye ameahidi kuwa kampuni yake itajenga kiwanda kikubwa cha bia kitakachogharibu takribani dola milioni 100 za Marekani mkoani Dodoma.

Bw. Jarrin ameeleza kuwa hatua hiyo inalengo la kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Amesema kuwa mafanikio makubwa ambayo kampuni yake imeyapata hapa nchini hasa baada ya kubadilisha ujazo wa kinywaji chake kimoja umeifanya Kampuni yake ifikirie kuongeza uzalishaji kwa kuongeza kiwanda kingine mkoani humo.

Bw. Jarrin amebainisha kuwa upanuaji wa huduma zake nchini utakwenda sambamba na kuendeleza kilimo cha mazao yanayotumika kutengenezea vinywaji hususan shayiri ama ngano hatua ambayo itawanufaisha wakulima nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameuelezea mpango huo wa TBL kwamba utachochea ukuaji wa uchumi na ajira kwa wananchi.

“Tunataka kujenga Tanzania ya viwanda, na TBL ni kiwanda ambacho kitanipa ajira kwa Watanzania, kitanipa kipato zaidi, lakini pia nataka Dodoma iwe kitovu kingine cha uchumi kwa kutupatia mapato kama ilivyo Dar es Salaam inayochangia zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya Serikali” alisema Dkt. Mpango.

Ameunda timu ya wataalamu itakayopitia na kuchambua masuala mbalimbali ya kikodi na kisera yaliyowasilishwa na kampuni hiyo ili yafanyiwekazi haraka kwa manufaa ya pande hizo mbili.

“Ameahidi kuwekeza kiwanda chenye thamani ya Dola milioni 100 na ili aweze kufanya hivyo amehitaji ajue msimamo wa Serikali kuhusu kupunguza gharama za uendeshaji ikiwemo kodi na mambo mengine ambayo tutayafanyiakazi” Alisisitiza Dkt. Mpango

Dkt. Mpango amesema kuwa ameweka utaratibu wa kukutana na wawekezaji wengine wanaozalisha vinywaji baridi na vikali ili kufungua wigo zaidi wa majadiliano ili kukuza uwekezaji hapa nchini kwa kuangalia na kujadiliana kuhusu vikwazo na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *