Habari Kitaifa

Ukatili wa Kijinsia Mila na Desturi Zenye Madhara kwa Watoto Bado Changamoto katika Malezi

on

Dunia ikielekea kuadhimidha Siku ya Familia Duniani Mei 15, 2018, watoto 13,457 wameripotiwa kufanyiwa ukatili hapa Nchini.

Hayo yamesema na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa mdahalo wa siku moja kujadili masuala ya familia na malezi kwa Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii na wadau wa masuala ya watoto leo jijini Dodoma.

Mhe. Ummy amesema takwimu hizo ni matokeo ya taarifa ya Jeshi la Polisi Nchini kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2017 peke yake.

Waziri Ummy  ameimbia Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii pamoja na wadau wa masuala ya watoto kuwa familia ni chimbuko la uzalendo, maadili ya kitaifa, umoja, amani,na mshikamano na ni chanzo cha nguvu kazi kwa Taifa.

Ameongeza kuwa familia nyingi hapa nchini bado zinakabiliwa na changamoto  ya mila na desturi zenye madhara na ukatili wa kijinsia kwa watoto ndani ya familia.

Wakati huo huo Kaimu Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Marcel Katemba amesisitiza kuwa malezi bora ni muhimu katika Ustawi wa Jamii nchini hivyo wazazi wana wajibu wa kutoa malezi bora kwa watoto wao.

Kwa upande wake Mtoa Mada Katika mdahalo huo Mhadhiri kutoka Chuo cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE)  Dkt.  Hezron Onditi amesema kuwa utafiti uliofanywa na taasisi yake unaonesha kumekuwa na vitendo vya ukatili wa kwa watoto katika mtandao na hii inatokana na malezi duni ya baadhi ya wazazi katika familia. 

Aidha takwimu zinaonesha kuwa kwa Dunia nzima watoto 72% wamepata ukatili kwa njia ya mtandao na watoto 44% duniani wamekili kuwakatili wenzao kimtandao.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Uwekezaji katika watoto na Jamii zao (ICS) Bw. Kudely Sokoine amesema kuwa wanaume wana mchango mkubwa katika kuleta msingi bora wa malezi Katika familia. 

Naye mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii Mbunge wa Urambo Mhe. Magreth Sitta amesema kama ukioa au kuolewa uku ukiwa na mpango wa kuachana na mkeo/mme basi  usioe.

Mdahalo huu umeandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika Kimataifa Plan Tanzania kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya  Familia duniani ambayo hufanyika kila tarehe 15 mwezi Mei na yataadhimishwa katika ngazi ya mkoa nchini kote. 

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *