Habari Kitaifa

Walimu wa Shule za Sekondari wapatiwa Mbinu za Kupambana na Ukatili wa Kijinsia

on

Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendeleza juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni kwa kuwawezesha walimu wa shule za sekondari kwa kuwapa mbinu za kupambana na vitendo hivyo  katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Bi. Magreth Mussai alipokuwa akifunga mafunzo ya kupambana na ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni yaliyoandaliwa na walimu wenyewe kwa kushirikiana na Serikali na shirika la Femina.

Bi. Magreth Mussai amesema kuwa katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia Serikali ilizindua Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Jinsia wa mwaka 2017/2018 hadi  mwaka 2020/2021.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza Mpango mkakati wa Kupambana na ukatili wa kijinsia Wizara ilianzisha  kampeni ya kutokomeza ndoa na mimba za utotoni iliyozinduliwa na Wizara hivi karibuni Mkoani Mara inayosema: “Mimi ni Msichana Najitambua na Elimu ndio Mpango Mzima”  

Kwa upande wake Meneja wa Uhamishaji wa Femina Bi. Nashivai Molleli  amesema kuwa elimu walioyoitoa kwa walimu walezi hao itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa weledi na uadilifu kama walezi wa wanafunzi shuleni katika kupambana na ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni kwa kutoa elimu kwa wanafunzi, walimu, kamati za shule na jamii kwa ujumla.

Naye Mwalimu Mlezi wa  Shule ya Sekondari Mnelo ya mkoani Lindi Bw. Adam Matimbwa amesema kuwa  wao kama walimu walezi katika shule elimu walioipata ni muhimu sana kwao katika kuwapatia uelewa, maarifa, mbinu, na stadi za kumlinda mtoto wa kike,

“Tunataka kuamsha ari ya wavulana kuwalinda wasichana wanaosoma nao, na kuwa mabalozi wa kushauri na kutoa elimu kwa makundi mengine wengine hasa wakiwemo walimu na vijana wa mitaani kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni katika maeneo yao ya kazi, jitihada hizi zinalenga kupunguza na kutokomeza kabisa aina hizo za ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/2022” alisema Bw. Matibwa.  

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *