Uchumi Zone

Wamachinga Watakiwa Kuchangamkia Fursa ya Kujisajili na Kupatiwa Vitambulisho

on

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi hususani wamachinga kujisajili na hatimaye kupatiwa vitambulisho maalum kwa lengo la kusaidia biashara zao kutambulika, kukopesheka na kurahisisha mawasiliano ya usimamizi wa biashara hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo uliofanyika leo mkoani Arusha, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Fabian Daqqaro amesema ni muhimu wafanyabiashara kutumia fursa hii ya kujisajili ili kurasimisha biashara zao.

“Ni matumaini yangu kuwa, wafanyabiashara wengi wadogo wadogo mkoani hapa, mtatumia fursa hii kujisajili kwa sababu ninafahamu wengi wenu malengo yenu siyo kuwa wafanyabiashara wadogo muda wote, bali mtakuza biashara zenu na kuwa wafanyabiashara wakubwa na hii itawezesha kuchangia mapato ya Serikali,” alisema Daqqaro.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Abdul Zuberi ameeleza kuwa, zoezi hili la kuwasajili na kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara wadogo limetokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

“Ni ukweli usiopingika kwamba,  Rais wetu kwa nyakati tofauti amekuwa akiwapigania na kutaka wafanyabiashara wadogo wadogo kutambulika rasmi na kupatiwa vitambulisho ikiwa ni pamoja na kutafutiwa maeneo rafiki ya kufanyia biashara zao,” alisema Zuberi.

Ameongeza kuwa, kutokana na juhudi hizo za Rais Magufuli, Serikali kupitia Kikao cha Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, ilifanya marekebisho mbalimbali ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi na jukumu hili limekasimiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Zuberi alisema kuwa, zoezi hili limeshafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza na sasa limefanyika mkoani Arusha ambapo jumla ya vikundi 125 vya wafanyabiashara wadogo vinatarajiwa kusajiliwa na hadi sasa vikundi 25 vimeshatambuliwa  vikiwa na jumla ya wafanyabiashara wadogo takribani 3,600 na kwa uwakilishi wafanyabiashara 100 wamepatiwa vitambulisho jijini hapa.

Naye Kiongozi wa Wamachinga mkoani Arusha Fredson Athumani, ameishukuru Serikali kwa kuwatambua rasmi na kusisitiza kuwa, atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake pamoja na Serikali kuwahamasisha wafanyabiashara wote wadogo kusajiliwa na kupata vitambulisho maalumu.

Zoezi la usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi linafanyika chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Serikali za Mitaa, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *