Habari Kitaifa

Wananchi wa Liwale na Nachingwea walilia Barabara

on

Wananchi wa Wilaya ya Liwale na Nachingwea  mkoani Lindi wameiomba Serikali  kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara ya Liwale – Nachingwea yenye kilomita 129 kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za usafirishaji wa abiria  na mazao katika wilaya  hizo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, Mkuu wa wilaya ya Liwale Bi. Sarah Chiwamba amesema kuwa wananchi wake wanaamini kuwa Liwale itafunguka kibiashara na kiuchumi endapo itakuwa imeimarishwa katika mtandao wa barabara ambazo zitaiunganisha wilaya hiyo na  wilaya jirani pamoja na nchi kwa ujumla.

“Naamini barabara hizi zikikamilika wilaya hii na mkoa wetu utaendelea kiuchumi kwani suala la miundo mbinu ya barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu  katika wilaya yetu.” amesema Bi Chiwamba.

Aidha Bi. Chiwamba amefafanua kuwa wananchi wengi katika wilaya hiyo ni wakulima hivyo wamekuwa wakitumia miundombinu ya  barabara kusafirisha mazao ya korosho na  ufuta yanayozalishwa kwa wingi kuelekea maeneo  mbalimbali ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Kwandikwa anayeshughulikia masuala ya Ujenzi, amewataka wataalamu wote wa masuala ya ujenzi nchini kupitia Sera ya ujenzi ya mwaka 2003 ambayo itawasaidia kuwapa mwongozo katika utekelezaji wa majukumu yao katika kutoa huduma bora kwa jamii.

Ameongeza kwa wataalamu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuwa wabunifu katika  ujenzi wa barabara zao ili kuondoa dhana  potofu iliyopo dhidi  ya usimamizi  wa barabara kati  yao  na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

“TANROADS na TARURA shirikianeni katika  kuhakikisha mnawajengea wananchi miundombinu iliyo bora, kusiwepo na utofauti kati ya barabara mnazo zisimamia.” alisema Mhe. Kwandikwa.

Ametoa wito kwa uongozi wa TANROADS mkoani  Lindi kuhakikisha kuwa  wanaboresha maeneo yote ya barabara ambayo ni korofi ili yaweze kupita kiurahisi katika kipindi chote cha mwaka.

Naye Meneja  wa TANROADS mkoani Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuendelea na mpango wa matengenezo ya barabara kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa mbalimbali katika mkoa huo. 

Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika  ziara  ya kikazi mkoani Lindi kujionea hali halisi ya mtandao wa barabara katika mkoa huo ambapo pamoja na mambo mengine ametembelea na kukagua daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo kwenye mto Lukuledi katika  barabara ya wilaya ya Luchelegwa – Ndanda inayounganisha wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi  na Masasi mkoa wa Mtwara ilikujionea miundombinu yake.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *