Viwanjani

Wasanii watakiwa Kutengeneza kazi Zzuri itakazovutia Wadhamini

on

Serikali imewataka wasanii kutengeneza kazi nzuri zenye ubora zinazozingatia maadili ya Kitanzania ili kuwavutia wawekezaji wengi wanaotaka kudhamini kazi  hizo katika kuziandaa na kuzisambaza.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe wakati akizindua Mfumo wa MaxBurudani ulioandaliwa  na Kampuni ya MaxMalipo ambapo ameishukuru Kampuni hiyo kwa kuamua kuchukua dhamana ya kusambaza kazi za wasanii ili kuondoa kero ya muda mrefu ya wizi wa kazi za wasanii hao kupitia njia mbalimbali walizokuwa wanatumia wasanii hao ambazo zilikua zikiwalipa kiasi kidogo.

“Nimefurahishwa sana na Mfumo huu namna ambavyo utaweza kutatua changamoto ya wizi wa kazi za wasanii wetu kwa vile umeonyesha wazi namna ambavyo msanii anaweza kunufaika na kazi yake kuanzia idadi ya kazi zake zilizoenda sokoni,asilimia anazopata kwa kazi yake ambayo ni kuanzia 40-50 pamoja na kumuwezesha kutouza Haki Miliki yake kama walivyokuwa wanafanya hapo awali.” alisema Dkt. Mwakyembe.

Aidha amewataka Wasanii kutengeneza kazi zenye ubora ambazo zitakidhi vigezo vyinavyotakiwa na Kampuni hiyo ambapo pia ameiagiza Kampuni hiyo kutochukua kazi yeyote ambayo itakuwa haina ubora wala kuwa na maadili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Mhandisi James Kasati amesema kuwa Mfumo wa MaxBurudani inalengo la kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao kwa kuwa ndio kundi lililoajiri vijana wengi hapa nchini.

Mhandisi Kasasi ameongeza kuwa Mfumo huu utatumia mawakala wa Max Malipo katika kusambaza kazi hizo ambapo Msanii atatakiwa kupeleka kazi ambayo itakuwa imekidhi vigezo vya kusmbazwa na Kampuni hiyo ndani na nje ya nchi kwa zile nchi ambazo Kampuni hiyo ina matawi.

“Mfumo huu utatumia teknolojia katika kusambaza kazi za wasanii,kulinda Haki Miliki za Wasanii lakini pia msanii kujua takwimu sahihi za mchanganuo wa kazi yake pamoja na namna ambavyo anaweza kulipa kodi kwa Serikali”.Alisema Mhandisi Kisati.

Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bibi.Joyce Fissoo amesema kuwa Bodi yake inapokea Kampuni au mtu yeyote ambae anataka kusambaza kazi za wasanii endapo tu atakuwa anawalipa Wasanii hao kile wanachostahili kupata kupitia kazi hizo.

Aidha Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Muingereza mbali na kuipongeza Kampuni hiyo kwa Wazo zuri lakini pia ameishauri kuona ambavyo inaweza kuwasadia wasanii hao kupata  mikopo itakayowasaidia kuandaa na kutengeneza kazi nzuri.

Mfumo huo tayari umeanza kupokea baadhi ya kazi za wasanii tayari kwa kuzisambaza ambazo ni Filamu ya Kampuni ya J For Life, Albamu ya Fiesta  pamoja na Albamu ya Msanii wa Nyimbo za Injili Bw. Godluck Gosbert.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *