Habari Kitaifa

Waziri Mkuu MAJALIWA “Vita Dhidi ya Rushwa, Serikali yaokoa Shilingi Bilioni 53.9”

on

Waziri Mkuu KASSIM MAJALIWA amesema Serikali imefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizochukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika mwaka 2016/2017.

Amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno ikilinganishwa ni shilingi bilioni 7.0 tu ambazo ziliokolewa katika mwaka 2015/2016.

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 9, 2017) wakati akifungua semina ya Mtandao wa Wabunge  wa Afrika walio katika Mapambano ya Rushwa (APNAC) tawi la Tanzania kwenye ukumbi wa African Dream mjini Dodoma.

Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza kupata mrejesho mzuri kwamba watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea kupungua. 

“Baadhi ya hatua tulizochukua ni  pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya TAKUKURU; kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza mianya ya kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia nidhamu katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” amesema.

Amewaomba wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali kwani haina mzaha kwenye mapambano hayo. “Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya rushwa na tutaendelea na mapambano hayo. Hivyo, ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono katika mapambano haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono kwenye vita hii,” amesisitiza.

Waziri  Mkuu  Kassim  Majaliwa  akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Utumishi na Utawala Bora Anjela  Kairuki  ,baada ya kufungua Semina  ya Mtandao wa Wabunge wa Africa Tawi la Tanzania  walio katika Mapambano  Dhidi ya Rushwa (APNAC) katikati ni Naibu Spika  Dr Tulia Apsoni, Semina hiyo ya siku mbili inafanyika Mkoani Dodoma katika ukumbi wa Hoteli ya African Dreams . June 9, 2017 na June10,2017 nakuendeshwa na UNDP.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akisalimina na Mshauri wa Maswala ya Bunge  kutoka ofisi ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa  Tawi la Tanzania ,Bibi Anna Hovhannesyan , baada ya kufungua Semina  ya Mtandao wa Wabunge Africa Tawi la Tanzania  walio katika Mapambano  Dhidi ya Rushwa (APNAC) Semina hiyo ya siku mbili   inafanyika Mkoani Dodoma katika ukumbi wa Hoteli ya African Dreams . June 9, 2017 na June10,2017 nakuendeshwa na UNDP.

About Habari360_1

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *