Uchumi Zone

Waziri Mpango Ateta na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO

on

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo ya viwanda (UNIDO), Bw. Li Yong ambapo wawili hao wamezungumzia namna Tanzania na UNIDO zinavyoweza kuimarisha zaidi ushirikiano ili kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2015.

Katika mazunguzmo hayo Dkt. Mpango amesema Serikali ya Tanzania inathamini sana mchango wa kitaalamu unaotolewa na shirika hilo, hasa katika mipango ya maendeleo ya kiuchumi, na kuwataka kuendelea kuiunga mkono Serikali hasa katika kusaidia uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ili kuinua sekta ya viwanda.

“Katika miaka mitano ya kwanza ya mpango wa maendeleo wa Taifa, mojawapo ya agenda ni kuboresha miundombinu, nishati ya umeme, teknolojia ya mawasiliano na rasilimali watu ambapo vyote kwa pamoja vitatufikisha katika malengo tuliyokusudia”  alisema Dkt. Mpango.

Aidha Dkt. Mpango amesema sekta ya viwanda ni sekta muhimu, hivyo Serikali inahitaji kushirikiana kwa pamoja na wadau mbalimbali ili iweze kufikia malengo iliyojiwekea katika miaka mitano ya kwanza ya mpango wa maendeleo wa Taifa.

“Mpango wa maendeleo wa sasa unalenga kuifanya nchi yetu iwe nchi ya uchumi wa kati, kwa kujenga mazingira mazuri ya biashara na kuzalisha wataalamu wa viwandani” Alisisitiza Dkt. Mpango

Alisema kuwa pamoja na mikakati hiyo ya kuendeleza viwanda bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikwemo ya uzalishaji mdogo wa bidhaa za viwandani, uzalishaji wa bidhaa ambazo hazikidhi ubora wa kimataifa na uchache wa wataalamu katika usimamizi wa shughuli za viwandani, hivyo Serikali inahitaji kuungwa mkono na  sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta ya viwanda.

Kwa upande wake Bw. Li Yong, amesema ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali, ni lazima kusimamia vyema maono na mikakati ya kimaendeleo na kuongeza kuwa anatarajia kujifunza vitu vingi kipindi atakchokuwepo hapa Tanzania, hasa katika hatua ambayo nchi  imefikia katika uendelezaji wa viwanda.

Li Yong alisisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi na kupanga mipango thabiti itakayoiwezesha sekta hiyo kukuza uwekezaji kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara na kuahidi kuwa Shirika lake liko tayari kufanikisha azma hiyo ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *