Habari Kitaifa

Wizara ya Madini Kutotoa Leseni kwa Mwekezaji Mbabaishaji

on

Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kuwa Wizara yake  haitatoa leseni ya uchimbaji madini kwa mwekezaji aliyepewa leseni ya kuchimba  madini katika  eneo la kijiji cha Ishokelahela  wilaya ya Misungwi baada ya kushindwa kuendeleza eneo hilo kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.

Akiwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa wilayani humo,  Nyongo alisema kuwa mwekezaji huyo alipewa leseni ya uchimbaji wa madini kwa kipindi cha miaka 10 na hakuna uendelezaji wowote  alioufanya katika machimbo hayo.

Uamuzi huo umetokana  na malalamiko  ya  wananchi  wa  kijiji  hicho  wakati wakitoa dukuduku zao kwa Waziri Mkuu kuwa, mwekezaji  huyo amekuwa akiwazuia wachimbaji wadogo kuchimba madini katika machimbo hayo hali iliyopelekea Waziri Mkuu kumtaka Naibu Waziri wa Madini kulitolea ufafanuzi suala  hilo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mwekezaji huyo, Mhe. Nyongo alisema kuwa  kutokana  na kutoendeleza machimbo hayo mwekezaji huyo amekuwa  haelewani na jamii inayozunguka machimbo hayo na kwamba  hapo  awali  wananchi walikuwa wanafanya shughuli za  uchimbaji katika  katika eneo hilo kabla ya kupewa mwekezaji huyo.

‘’Mwekezaji huyu anayefahamika kwa jina la Badir Soud kwa kuwa leseni yake imeisha na ameomba tena leseni hiyo ya uchimbaji hatutampa, na sisi kama Wizara ya Madini tutawapatia wananchi wachimbe wakiwa katika mfumo wa vikundi’’ alisema Mhe. Nyongo.

 Aliendelea kueleza kuwa,  pamoja na kutokuendeleza mgodi huo katika kipindi hicho,  mwekezaji huyo hajapeleka vifaa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji katika eneo la mgodi jambo ambalo linaikosesha Serikali mapato.

Naibu Waziri Nyongo alitumia fursa hiyo kuwaagiza wachimbaji wa madini nchini kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria  za uchimbaji madini  ili waweze kutambulika rasmi na kuweza kulipa kodi serikalini.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *