Habari Kitaifa

Wizara ya Maliasili na Utalii Yakabithiwa Rasimu ya Mwisho ya Sera ya Taifa ya Misitu

on

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekabidhiwa rasimu ya mwisho ya sera ya Taifa ya Misitu na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)  kufuatia kukamilika kwa mchakato uliowashirikisha wadau wote muhimu.

Hatua hiyo inafuatia ikiwa ni mwaka mmoja sasa ambapo FAO na wizara ya Maliasili na Utalii ziliposainiana mkataba wa msaada wa Kitaalamu kuisaidia serikali kukamilisha Mapitio ya Sera ya Taifa  ya Misitu ambayo ilipitishwa mwaka 1998.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi  amesema  Tanzania inakabiliwa changamoto katika kuthibiti rasilimali misitu kwa kuwa sera ya misitu inayotumika kwa sasa ni ya zamani hali inayochangia kushindwa kuendana na kasi ya  maendeleo  sasa.

Ameyasema hayo leo katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika makao makuu ya ya Wizara mjini Dodoma baina yake, na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) hapa nchini, Fred Kafeero.

Maj. Gen. Milanzi amesema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka wakati ambapo nchi inakabiliwa na changamoto nyingi za uharaibifu wa misitu.

‘’Tunahitaji sera dhabiti ya kukabiliana na masuala mbalimbali yanayohusu uharibifu wa rasilimali za misitu’’ alisisitiza Milanzi.

Kwa upande wake, Kafeero alisema alisema FAO imepiga hatua kubwa za mafanikio katika kukamilisha  mchakato wa kuandaa rasmu hiyo ambayo ni shirikishi.

‘’Tayari FAO imesaidia nchi nyingi kwenye maeneo hayo lengo likiwa kuhakikisha kuwa sera hiyo inatilia maanani masuala ya maendeleleo ya kitaifa na kimataifa.

Aidha, Kafeero alisema misitu ni moja ya maeneo ya majukumu makuu ya FAO kwa kuwa ni moja ya maeneo muhimu yanayohusiana na matumizi endelevu ya maliasili, uhakika wa chakula na lishe pamoja na maendeleo ya uchumi kwa ujumla.

Wakati huo huo, FAO pamoja na Serikali wanamalizia taratibu za kuandaa mkakati wa kuitekeleza  Sera hiyo ili  iweze kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa katika misitu nchini.

 

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *