Habari Kitaifa

Chanjo ya Kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi Kuanza Kutolewa Februari 23

on

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amezindua zoezi la utoaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 linalotarajiwa kuanza siku ya jumatatu Februari 23.

Akizungumza leo jijini hapa wakati akifungua semina ya chanjo hiyo iliyowashirikisha waandishi wa habari, wataalamu kutoka Wizara ya afya, pamoja na viongozi wa dini, Makonda amesema zoezi hilo ambalo linatarajiwa kuhusisha zaidi ya wasichana 2,497 mpaka kufikia mwezi  wa tano ambao watapatiwa chanjo katika vituo 270 ikiwemo shule na mitaa huku lengo likiwa kusaidia kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii ili kusaidia wasichana wajitokeza kwa wingi katika zoezi ili kupata chanjo hiyo.

Aidha Makonda amesema utoaji wa chanjo hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ukisababisha vifo vya kinamama wengi huku akiitaka jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara huku akitoa wito kwa viongozi wa dini, madiwani, wenyeviti  serikali wa mitaa na wajumbe kuhamasisha wananchi kwenda kupata chanjo hiyo.

“Kuna kasumba kuwa saratani ya tezi dume inapimwa kwa kidole jamani siyo kweli, kuna kipimo cha damu na ni rahisi hivyo nina mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba katika mkoa wangu kuhakikisha tunapima saratani hii kwa kina baba na kupunguza kasi  ya vifo kwa kinababa inapungua kwa kuwagundua mapema na kuwaanzishia matibabu,” amesema Makonda.

Hata hivyo amesema chanzo cha ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na mapenzi katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuzaa watoto wengi pamoja na uvutaji wa sigara ambapo dalili zake ni kutokwa na damu bila mpangilio, maumivu ya mgongo, miguu, kiuno, kutokwa na uchafu ukeni pamoja na kuchoka, kupungua uzito na hamu ya kula na kusema kuwa  Saratani ya mlango wa kizazi inasababishwa na virusi vya Human Papilloma ambapo kinga yake kwa hatua ya mwanzo ni kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini dalili za mwanzo na kupata matibabu stahiki.

Chanjo ya Saratani ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa mwaka 2018 itatolewa kwa wasichana wanaotimiza umri wa miaka 14 ambao wamezaliwa kuanzia Januari 01 hadi Disemba 31 mwaka 2004.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *